MUM News and Events

MUM kuanzisha kozi maalum kusaidia maendeleo ya Taifa

Posted on: 03 September, 2020

Katika kuhakikisha kinatoa wanafunzi wenye weledi katika kukuza uchumi wa Taifa, Chuo kikuu cha Waislamu cha Morogoro kinataraji kuongeza kozi mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya jamii katika Nyanja mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo septemba 2 mwaka huu na Makamu Mkuu wa Chuo hicho upande wa Utawala na fedha Profesa Musa Asad alipotembelea maonesho ya 15 ya  Vyuo vikuu  nchini yanayoendelea katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.

Profesa Asadi amesema Chuo kimeangalia mahitaji ya Taifa katika wakati huu ambao nchi ipo katika uchumi wa kati hivyo inahitaji wataalamu wa fani mbalimbali ambazo zitakuwa sababu ya kukuza uchumi  kuelekea viwango vya juu.

Amesema,  kozi  za Afya ni miongoni  mwa kozi zitakazoongezwa kutoka zile zilizopo sasa ili kuongeza wataalamu zaidi katika fani hiyo lengo likiwa kumsaidia Mtanzania kuondokana na uhitaji wa kusafiri nje kupata matibabu.

Pamoja na hayo Profesa Asad amesema Chuo hicho kipo katika mkakati wa kuwa kinara katika utunzaji wa mazingira ambapo kuna mpango maalumu wa kugeuza taka zinazozalishwa chuoni hapo kuwa mbolea itakayotuika kukuzia miche itakayooteshwa na chuo hicho.