MUM YATOA TUZO YA HESHIMA KWA PROF. LODHI
Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM kimetoa tuzo maalum kwa Mwanataaluma nguli Prof. Abdulazizi Lodhi ikiwa ni kutambua mchango wake katika kukuza Lugha ya Kiswahili.
Prof. Lodhi Mtanzania anayeishi nchini Sweden akifanya kazi zake za Kitaaluma, kwa miaka mingi amekuwa akifanya tafiti tofauti kutafuta asili ya maneno mbalimbali ya Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
Akiwa Chuoni MUM kwa ziara ya Kitaaluma Disemba 3, 2025, Prof. Lodhi kabla ya kukabidhiwa tuzo hiyo, amepata fursa ya kuzungumza na walimu kutoka Idara ya Lugha ya Kiswahili na kusisitiza umuhimu wa kufanya tafiti ili kufahamu asili ya maneno yanayotumika katika Lugha hiyo.
Prof. Lodhi amepokelewa Chuoni hapo na Mwenyeji wake Prof. Hamza Njozi ambaye ameitaja ziara hiyo ya nguli wa masuala ya Fasihi kuwa ni heshima kwa Chuo hicho.