INDONESIA YAIFIKIA MUM KWA KISHINDO
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Tri Yogo Jatmiko amewataka wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM kutumia fursa ya ushirikiano uliopo baina ya Taifa hilo na Chuo hicho kujiendeleza katika fani mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kuwasili Chuoni hapo kwa ziara maalum Disemba 6, 2025, Balozi Tri amesema yupo tayari kudhamini kazi yoyote ya utafiti ambayo itamhitaji mfanyakazi kutoka MUM kwenda kuifanya Nchini Indonesia kutokana na mada atakayoichagua.
Katika mazungumzo yake ya takribani saa mbili amewataka wafanyakazi wa chuo hicho kutumia fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa na Indonesia kujiongezea taaluma zao kwani fursa hizo ni za kweli.
Amesema Nchini Indonesia zipo Taasisi kubwa zinazotambulika Duniani ikiwemo taasisi ya Muhammadiyya inayopokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali na kuwafadhili katika masomo yao, na kuutaka uongozi wa chuo kushirikiana na Taasisi hizo ili kujitanua zaidi katika shughuli zake.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Prof. Hamza Njozi, amemshukuru Balozi Tri kwa kutebelea Chuoni hapo na kusema kwamba MUM ipo tayari kushirikiana na Indonesia ili kutoa wataalamu bora kwa maslahi ya Mataifa yote.