MUM News and Events

Vyuo vikuu vyatakiwa kufanya tafiti zitakazosaidia Taifa

Posted on: 03 September, 2020

Vyuo vikuu nchini vimetakiwa kujikita katika kufanya tafiti zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa nchi ikiwa sambamba na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania.

Wito huo umetolewa leo Agost 2 mwaka huu  na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Leonard Akwilapo wakati akifungua rasmi maonesho ya 15 ya vyuo vikuu nchini yanayoendelea katika viwanja vya mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.

Profesa Akwilapo amesema lengo la Tanzania ni kujitosheleza kwa kuwa na wataalamu waliobobea katika fani mbalimali ili kusaidia nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Amesema watanzania wengi wamekuwa wakisafiri kwenda nje ya nchi kupata huduma mbalimbali ikiwemo ya afya jambo ambalo pakiwepo wataalamu wa kutosha wa fani hiyo raia wa kigeni ndiyo watakaokuja nchini badala ya watanzania kwenda huko.

Aidha Prof. Akwilapo amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za kuhakikisha wanafunzi wenye malengo ya kusoma wanatimiza ndoto zao kwa kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuongeza kiwango cha utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu nchini (TCU) Profesa Charles Kihampa ameishukuru Serikali kwa kushirikiana nao ili kuhakikisha wanafunzi wa Kitanzania wanatimiza ndoto zao za kielimu.

Maonesho ya 15 ya Vyuo vikuu nchini yameanza Agost 31 mwaka huu na kufunguliwa rasmi leo septemba 2 mwaka huu ambapo yanataraji kufungwa siku ya jumamosi ya septemba 5 mwaka huu.